Zangu Salamu ziwafikie Wanafunzi wote wa SAUT pale Nyakato Kwa Upendo wao Mwingi waliouonesha Kwangu kwa siku nilizokuwa hapo Chuoni Kwao. Kwa heshima ya Kipekee nimshukuru Adolf Nzwalla pamoja na wafanyakazi wa HCC Alive FM 91.9 Kwa masafa ya Mkoani Mwanza. Mlinifanya nikajisikia bado niko Dar, Mungu sio Filikunjombe Mwezi wa December, 2012 ratiba yetu iko kama Kawaida.
Ninamshukuru Mungu Kwa kuniwezesha leo Kuandika Papaa On Tuesday ya 44 kwenye mwaka huu nikiwa nimebakiza POT 8 kutimiza 52 Kufunga Mwaka 2012. Mungu ni Mwema sana kwa kila iitwapo leo.
Kaika Clip niliyoitupia hapo Juu utamsikia President Barroso akieleza Msemo wa Papaa On Tuesday Ya leo ambayo kwa mara ya kwanza Mwaka Jana mwezi kama huu November, niliandika POT yenye kichwa cha habari kama hiki cha leo. Gonga hapa kwa kumbukumbu isiyooza..http://samsasali.blogspot.com/2011/05/papaa-on-tuesdayif-you-want-go-fast-go.html.
Kati ya Mambo ambayo Watanzania na Waafrika tunapenda hasa ni Kukutana ama Vikao, hata kama kuna Option ya Technolojia lakini still watu wanapenda kukutana. Na Mnapokutana kuna kuwa mijadala mirefu ambayo mwisho wa siku unaweza mkakuta mnaarisha maamuzi mliyotaka kuafikiana sababu kumekuwa na lundo la mawazo.mnajikuta kwenye kikao mnaambiana 'Kila Mtu akatafakari Kisha alete Majibu". Badala ya Kukaa Kikao Kimoja mnajikuta mnakaa Vikao Vitatu. Ingawa kwenye wengi hapaharibiki neno lakini Wapishi wengi Huaribu Mchuzi.
Kuna baadhi ya mambo kwenye maisha ukitaka kufanya na watu wengi na kushirikisha watu wengi utajikuta uko pale pale badala ya kusonga mbele hasa mambo ya maendeleo. Kuna baadhi ya mambo basi amua mwenyewe amua kiume amua kujilipua utasonga. Miluzi mingi humpoteza Mbwa lazima ifike hatua uweze kuamua mambo ili uweze kwenda haraka. Sio Kila Mtu anaweza kuwa na mzigo na kile ulichonacho ndani ya moyo wako. Unaweza kuta wewe ndiye unayeingia gharama ya Muda, fedha na pengine hata maumivu ya nafsi sababu kuna mtu anataka kuamua hatma ya jambo fulani. Kuna nyakati kwenye maisha tumeruhusu kunyanyaswa kwa Mkataba wa Kujiona kuwa fulani anatakaiwa aamue kwa niaba yako. Unaweza kuta umemshirikisha mtu ama watu jambo fulani ambalo watu hao jambo hilo hawajalipa Uzito wewe uliolipa jambo hilo. Matokeo yake imepita wiki, miezi umeshindwa kuendelea mbele sababu tu unahitaji kufanya kwa pamoja. Kwa wale ambao tumewahi kuishi maisha ya "Gheto" ambako mnachanga Kununua Luku ama kama Mna share Luku na Mpangaji mwenzio na zamu yake ya kununua Luku imefika ghafla anakuambia hana hela siku hiyo swali la kujiuliza utasubiri zamu iende sawa ukae gizani ama uamue kununua Luku sababu una issue zako za msingi zinahitaji umeme. Jiulize kuna mambo mangapi tumehairisha kufanya sababu 'Wajumbe" wamekataa kupitisha hiyo idea wakati wewe still unaona kuna Mpenyo katika hilo wazo. Wakati mwingine ni vema watu wakaku-Join mbele ya safari baada ya kuamua kufanya wewe mwenyewe.
Ni kweli tunawahitaji watu katika maisha yetu, Ni kweli umoja ni Nguvu na ukweli ni kwamba watu wanatusaidia kwenda mbali zaidi, wanatusaidia kutuongezea mawazo, wanatusaidia kututia moyo tunapoamua kwa pamoja, Mkiwa wengi mnagawana hata maomivu ya kushindwa kwa jambo, Mkiwa wengi mnagawana hata hasara ya jambo na kwa sababu hiyo inakufanya ufanye sawa sawa na kundi linavyoamua na sio wewe unavyoamua katika maisha. Ukitaka kwenda mbali zaidi kwenye maisha nenda na watu ila kama unataka kwenda na speed ya kimaendeleo basi amua kufanya mwenyewe. Kuna kazi, mahusiano na hata biashara tumewahi poteza sababu ya opinion za watu. Wiki 2 zilizopita niliandika POT kuhusu Kusikiliza Sauti ya Ndani. Lazima uwaze nini unafanya na kwafaida ya nani na Kwanini unafanya.
Asilimia kubwa ya watu waliofanikiwa katika maisha ni watu walioamua kufanya pasipo kusubiri kila kitu kimekaa shwari, ukishaanza kuuliza uliza kwa watu jambo la kuamua leo itakuchukua wiki nzima kwa jambo ambalo una uwezo wa kuamua kwa haraka. Mbaya zaidi unakuta kwa sababu ya ushauri wa watu unachelewa kufanya maamuzi uliyotakiwa kufanya leo. Sikatai kupata maamuzi ya watu ni kweli utafika mbali sana, lakini ukitaka kufanya haraka basi unahitajika kujitwisha mslaba wako kila iitwapo leo.
If You want to go Fast Go Alone, If You Want To Go Far Go Together.