Kwenye kiswahili kuna methali, nahau na Misemo ambayo huwa inatupa
tafakari ya kina kuhusu maisha. Na hii misemo yote ni kwa ajili ya kutufunza
kile wahenga wanachodhani ni busara kwenye kizazi chao, Chetu na kinachokuja
kujifunza kutoka kwao katika yale waliyoyapitia. Kwenye mila za Kiafrika kuku
huliwa wakati wa sikukuu ama anapokuwa anakuja mgeni. Ukiacha siku hizi kwenye
huu ujio wa Kuku wa Kizungu enzi hizo wakati Nahau zinatungwa kulikuwa hakuna
wazo kama kuna Kuku aina nyingine watakuwepo duniani kila nyumba ilikuwa na
utamaduni wa kufuga kuku hasa kwenye jamii za wafugaji, inapotokea kuna ugeni
katika nyumba fulani basi ndio wakati muafaka sana wa kuku kuchinjwa. Katika
banda kulikuwa kuna jogoo na wale wanaotaga kwa ajili ya kutotoa kuongeza uzao.
Kuku wanaotaga walikuwa wanahifadhiwa kwa ajili ya manufaa ya baadae ndipo
wahenga wakasema "Kuku anayetaga huwa hachinjwi".
Kuna mambo kadha wa kadha ya kujifunza kupitia kuku wa kutaga na
suala zima la kuchinja kuku. Kuchinja ni kuondoa uhai wa kuku na kupoteza faida
ambazo mfugaji angeendelea kuzipata iwapo angeendelea kufuga yule kuku.
Tunachangamoto kubwa sana ya kujua kwenye maisha yetu nini ni kuku anayetaga na
lini pia achinjwe. Wengi tumekuwa tukichinja kuku anayetaga na kupoteza kabisa
dira za kwenye maisha. Fursa ambazo huwa zinakuja kwenye maisha yetu ni nadra
sana kuzirudia kwa sababu mbalimbali tumekuwa tukizipoteza ama kuziharibu kwa
kutokujua kuwa yamkini fursa hizo zingetusaidia kwa mambo mengine kwenye
maisha.
Mara kadhaa nimeongea kwenye hadhara ambazo nimekuwa na fursa ya
kuzungumza kuhusu Kizazi tulichonacho kisivyoweza kuziona na kuzithamini fursa
tulizonazo. Wengi wetu ni ngumu kuzikabiri changamoto tunazokutana nazo kwenye
maisha iwe ajira, iwe mahusiano, iwe kitaaluma iwe chochote kile kizazi hiki
tumejifunza kuchukua maamuzi ya hasira kuliko busara, wengi tunaamini tunaweza
ishi bila yeyote,na tunaweza fanya chochote pasipo msaada wa yeyote mwisho wa
siku tunakwama kwenye mambo mengi kwa sababu tulidhani sisi ndio kila kitu.
Ndio maana leo mtu akiwa na hasira anaweza ukashangaa alikuwa anafanya kazi
kutokana na namna moja ama nyingine anakasirishwa na mazingira ya kazi anaamua
kuongea yote, anafunguka kupita maelezo utamsikia "kazi itakuwa hii bana,
kazi zipo za maana, kaofisi gani haka" anaongea mwisho wa siku anaamua
kuacha anarudi nyumbani hasira zikiisha anagundua kuwa alitukana Wakunga wakati
uzazi ungalipo alimchinja kuku anayetaga tena kwa kisu butu.
Maamuzi ambayo tunayafanya kwenye maisha hutugharimu iwapo
hatutajua matokeo ya maamuzi hayo maana tunao uwezo wa kuchagua nini cha
kufanya hila hatuna uwezo wa kuamua namna ya matokeo iwapo tu matokeo
yanajulikana na unapaswa ukubaliane nayo. Unao uwezo wa kuchinja kuku anayetaga
ama asiyetaga. Asilimia kubwa ya watanzania tunaishi katika nyumba za kupanga
unaishije na majirani zako, unaishije na watu wanaokuzunguka. Mkorofi hana dini
wala kabila dini yake na kabila lake ni Ukorofi. Ukiona majirani
hawakushirikishi katika mambo yao mengi ujiulize unaishije na walimwengu.
Ukitaka kujua kipimo kidogo cha wewe unavyoishi na walimwengu subiri ikifika
jambo lako uone walimwengu watalipokeaje na kulichangamkia kiasi gani. Kama
wewe kila msiba uko busy ama kila mambo ya wenzio uko busy basi subiri ya kwako
yakifika na ukagundua unawahitaji watu wawe na wewe. Biblia inasema unavyotaka
watu wakufanyie wafanyie wewe kwanza. Jirani na nilipokuwa nikiishi Block 41
enzi hizo kulikuwa na mdada ambaye alikuwa na gari yake full tinted, anaweza
akapita kijiweni wala asisalimie ingawa salamu haipotezi chochote, anaweza
akakukuta barazani atataka wewe ndiwe umuanze alikuwa anajua hawahitaji wale
watu wa mtaa ule yeye level nyingine siku ya siku gari lake likaingia kwenye
mtaro, dada wa watu akashindwa kushuka kwenye gari akahangaika mwisho akashuka
watu wamekaa kwenye vibaraza vyao wanamtazama, akaenda kuomba vijana wa
kijiweni wamsaidie wakamuuliza "hivi leo ndo unajua sisi ni
watu"??pamoja na kutangaza angetoa fedha watu wakamkatalia, akadhani
atashinda vita ya wema kwa nyodo akachukua simu akampigia boyfriend wake aje
nae alipofika hakuwa na msaada ikabidi apige kaka wa watu aombe radhi kwa niaba
ya mpenzi wake ili kupata msaada wa kusukuma gari lile, ajabu wale vijana
wakasukuma gari na wakakataa kuchukua hela, tangu siku ile maisha ya mdada
yalibadirika salamu mbele kama skafu ya Chama Cha Maskauti.
Kwanini tufanya maamuzi ambayo hata kama yatatugharimu baadae
lakini tuchague kwa busara. Kwanini kuvunja simu ya mumeo au mpenzio kwa sababu
eti umekuta sms usizozielewa. Kwani tatizo ni simu ama ni mtu wengi tunapambana
na matokeo ya tabia tukidhani tunadhibiti chanzo cha tabia. Juzi kati nimesikia
kuna mtu amechoma gari la mumewe baada ya kukuta kwenye gari la mumewe kuna
Condom. Sasa ukichoma gari ndio unakuwa umemaliza tatizo la usaliti??Usiharibu
leo wakati unajua kesho utahitaji ama utawahitaji hao watu ama mtu. Kizazi
chetu ni kizazi cha Maamuzi ya hasira wapenzi wakikosana solution ya kwanza ni
Kuchuniana, baada ya masaa 600 ndio wanakuja kuanza kuongelea mgogoro wao wa
mapenzi. Kiwango cha kukabiriana na changamoto kinadhoofishwa na maamuzi wa
haraka haraka tunayoyachukua huku tukiwa bado tunauhitaji wa kile ambacho
tunataka kukipoteza leo. Tumechinja kuku anayetaga wa kazi zetu, tumechinja
mahusiano yetu, tumechinja biashara zetu wenyewe wakati bado tunavihitaji.
Idadi ya watu wanaoweza kuamini inazidi kupungua, kila mtu
anajihami na mwenzake kisaikolojia ama kivitendo kabisa, kwenye ajira mabosi wa
kikaburu na wafanyakazi wa kibongo full stress, wanandoa wanawake walishaamini
hakuna mwanaume ambaye ha-chit wote wanachit sema hatujui tu, wanachit kwa sms,
wanachit kingono, wanachit ki fedha, marafiki wanaoaminiana wako wachache wengi
wetu wanaishi bila na kuwa best friend, wengi wanaishi maisha ya wenyewe
wenyewe wakidhani wakikaa wenyewe ndio watakuwa salama zaidi. Nani anamwamini
nani kiasi cha kwamba akafunguka asilimia 500 hata wachungaji hawaaminiwi
itakuwa waumini. Ukimkopesha mtu fedha leo unaweka na asilimia za kuamini kuwa
utazungushwa kuipata hela yako. Kuna wengine kwa ajili ya kukopa kopa
wanashindwa kabisa kuaminiwa hata kama wanashida kubwa na ya ukweli. Kuna siku
walichinja kuku wa kutaga matokeo yake hana tena msaada kutoka kaw watu.
Ukifika saa ya wewe kukopa basi kila mtu atatoa sababu utasikia "yaani
sasa hivi hapa nimelipa ada".
Kila maamuzi unayoyachukua leo yatakugharimu either kwa heri ama
kwa shari. Ukiamua kuchinja kuku wa kutaga basi jua unapoteza kuku na mayai, na
vifaranga. Busara katika kuamua ndio msingi wa maendeleo. Inawezekana leo
ukaamua jambo ambalo wengi wasijue maana yake. Inawezekana una kuku mmoja ndo
huyo huyo ambaye anataga hata angekuja mgeni gani huwezi mchinja huyo kuku
sababu una hakika kabisa nikimuacha leo baada ya siku chache nitakuja kuwa na
kuku wengi. Maamuzi ya kutokuchinja ni maamuzi yako na sio maamuzi mepesi
lakini maamuzi ya kutokufanya sasa yana faida zaidi kuliko ukaamua kuchinja
leo. Kuna mambo mengi sana kwa sababu ya marafiki, sababu za tamaa zetu, sababu
za Kutafuta sifa kwenye maisha tumejikuta tumechinja Kuku anayetaga na kusahau
kuwa yamkini huyu kuku angetufaa baadae. Majuto ni Mjukuu wa Baba anayeitwa
maamuzi na mama anayeitwa wakati sahihi. Ukiamua jambo sahihi wakati sahihi
unaitwa una hekima kama sio busara, ukikosea hapo utakutana na majuto mtaa wa
mbele.
Kukua wa Kutaga Huwa Hachinjwi.
Ze Blogger
0798020110.
Papaa On Tuesday Kwa Hisani Ya Friends On Friday.